Lengo la kitabu hiki ni mtu kuwa na nukuu katika kila jambo katika kila hali katika kila kipengele cha maisha yake, kupata amani ya moyo na uhuru wa nafsi, kama msingi wa mafanikio, katika maendeleo ya maisha yake kwa ujumla wake.
Ukitaka kujitambua katika maisha yako jijibu maswali yafuatayo: Wewe ni nani? Umetoka wapi? Kusudi la maisha yako ni nini hapa duniani? Kisha tengeneza dira ya maisha ya nyuzi 360 inayozidi hata hatima ya maisha yako ya hapa.
Kitabu cha Falsafa za Enock Maregesi: Nukuu za Nyakati Zetu kitakusaidia kutengeneza dira ya maisha inayozidi maisha yako ya hapa duniani. Aidha, kitakusaidia kupata angalau nukuu 12 za kwako mwenyewe zitakazokuongoza na kukupeleka katika mafanikio yako ya kimwili na ya kiroho pia.
Mwandishi Enock Abiud Maregesi alizaliwa nchini Tanzania katika mkoa wa Mwanza mnamo mwaka 1972, Novemba 25. Alisomea teknolojia ya habari na utawala wa biashara katika Chuo Kikuu cha Wales, na uandishi wa habari na vitabu katika chuo cha fasihi ya ubunifu cha The Writers Bureau, nchini Uingereza. Alisomea pia sayansi ya roho ya Kabala katika Taasisi ya Bnei Baruch ya Petah Tikva nchini Israeli.
Mnamo mwaka 2015 kitabu chake cha kwanza, Kolonia Santita: Laana ya Panthera Tigrisi, kilishinda Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika; iliyotolewa na Chuo Kikuu cha Cornell cha New York, Marekani, na kampuni ya Mabati Rolling Mills ya Nairobi nchini Kenya. Anaishi jijini Dar es Salaam, Tanzania, anakojishughulisha na biashara na uandishi wa vitabu.
Kitabu kilihaririwa na Dkt Mathieu Roy aliyepata shahada ya kwanza ya falsafa ya chuo kikuu cha La Sorbonne, Paris, Ufaransa pamoja na shahada ya kwanza ya teknolojia ya habari baada ya masomo ya hisabati, biolojia, falsafa na teknolojia ya habari.
Alikutana na lugha ya Kiswahili, nchini Tanzania mwanzoni mwa mwaka 2000. Huba ya kujua Kiswahili ikampanda hasa upande wa mashairi na fasihi kwa jumla. Akapata shahada ya uzamili ya Kiswahili na shahada ya uzamivu ya Kiswahili kwenye Chuo Kikuu cha INALCO – Paris Sorbonne Cité. Tasnifu yake ya uzamivu inahusu kanuni za kutunga mashairi na ushairi wa Mathias E. Mnyampala. Anajishughulisha na uhariri wa vitabu vinavyoandikwa kwenye lugha ya Kiswahili, utafiti na teknolojia ya habari. Anaishi kati jiji la Paris na Dar es-Salaam, Tanzania.